Monday, October 18, 2010
Wachina kujenga mejengo ya kudumu ya 'Law School' Sam Nujoma
Wednesday, October 13, 2010
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA KATIBA NA SHERIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
RAIS KIKWETE AMTEUA JAJI OTHMAN CHANDE KUWA MWENYEKITI WA BARAZA LA UENDESHAJI WA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA –LUSHOTO
-------------------------------------------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Mhe. Jaji Othman Chande kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA). Mhe. Jaji Othman Chande ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Tanzania.
Rais amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 6(2) kikisomwa pamoja na ‘Schedule’ (1)(a) cha Sheria ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto, Sura ya 405.
Kufuatia uteuzi huo, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Mathias M. Chikawe (MB.), pia amewateua Wajumbe wengine 11 wa Baraza hilo. Mhe. Waziri amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa kifungu cha 6(2) cha Sheria ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto, Sura ya 405.
Uteuzi huu unafuatia kumalizika kwa muda uliowekwa kisheria wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Lushoto lililokuwa chini ya Uenyekiti wa Balozi Paul Rupia.
Uteuzi huu wa Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza la Uongozi la IJA-Lushoto umeanza tarehe 7 Agosti, mwaka huu (2010) na utakuwa wa baada ya miaka mitatu. Wajumbe wa Baraza la Chuo walioteuliwa ni:-
i. Mhe. Jaji Ernest Mwipopo (Mstaafu);
ii. Mhe. Jaji Aloysius K. Mujulizi, Mkuu wa Chuo – IJA ambaye atakuwa Katibu wa Baraza hilo;
iii. Prof. Palamagamba Kabudi, Mkuu wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
iv. Dkt. Eliuter G. Mushi, Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu Mzumbe;
v. Bi. Mary S. Lyimo, kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali;
vi. Bi. Asina Omari, Wakili wa Kujitegemea na Mwanachama wa Chama cha Wanasheria Tanzania Bara (Tanganyika Law Society);
vii. Bw. Francis Mutungi, Msajili wa Mahakama ya Rufani;
viii. Bi. Happiness P. Ndesamburo, Mkuu wa Kitengo cha mafunzo. Utafiti na Takwimu, Mahakama ya Tanzania;
ix. Bw. Mzee M. Mzee, Mhadhiri na Rais wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto;
x. Bw. Alex Benson, Mwakilishi wa Jumuiya ya Wafanyakazi IJA na;
xi. Rais wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto;
Mhe. Rais pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria wanawatakia Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Bodi mafanikio katika utekelezaji wa wa majukumu yao mapya katika kukitumikia Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto.
Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto kilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge No. 3, mwaka 1998 na kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Agosti, 2001. Chuo hiki kinatoa mafunzo ya Stashahada (Diploma) na Cheti cha Sheria kwa Wanachuo wanaotarajia kuwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Makarani katika wa Mahakama.
O.P.J. Mhaiki,
Katibu Mkuu,
Wizara ya Katiba na Sheria,
Makutano ya mtaa wa Mkwepu na Barabara ya Sokoine,
DAR ES SALAAM.